Hamia kwenye habari

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu jijini Strasbourg, Ufaransa

OKTOBA 11, 2024
HISPANIA

Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya Launga Mkono Haki ya Mashahidi wa Yehova ya Kuamua Matibabu Watakayopata

Mahakama Yamuunga Mkono Pindo Mulla Katika Kesi ya Pindo Mulla v. Spain

Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya Launga Mkono Haki ya Mashahidi wa Yehova ya Kuamua Matibabu Watakayopata

Septemba 17, 2024, Mahakimu wote wa Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu waliamua kwa pamoja kwamba haki ya mgonjwa ya kuchagua matibabu atakayopata kwa msingi wa imani yake ni lazima iheshimiwe. Kupatana na uamuzi huo muhimu, nchi ya Hispania na nchi zote 46 za Baraza la Ulaya zinahitaji kuheshimu haki ya mgonjwa ya kuchagua matibabu atakayopata.

Rosa Pindo Mulla na Armando, mume wake

Juni 2018, Dada Rosa Pindo Mulla, mwenye umri wa miaka 47, alilazwa kwenye hospitali moja jijini Madrid, Hispania, ili afanyiwe upasuaji mdogo. Awali kabla ya kupata matibabu, Rosa alikuwa amewapa madaktari wake kadi yake ya damu na akawaeleza kwamba imani yake na dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia haimruhusu kukubali kutiwa damu mishipani. (Matendo 15:28, 29) Wahudumu wa hospitali hiyo waliandika maagizo ya Rosa kwenye faili yake ya hospitali. Hata hivyo, hakimu aliwaruhusu madaktari wa Rosa kufanya upasuaji mkubwa na kumtia damu mishipani bila yeye kujua. Baada ya upasuaji huo, Rosa alihisi vibaya sana alipogundua kwamba wahudumu wa hospitali walikuwa wamepuuza uamuzi wake na kumtia damu mishipani, jambo ambalo alikuwa amekataa kabisa.

Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya lilipotoa uamuzi wake katika kesi ya Pindo Mulla v. Spain, mahakimu wote 17 walikubaliana kwamba “mgonjwa ambaye ni mtu mzima na ambaye ana uwezo wa kujifanyia maamuzi, ana haki ya kukataa” matibabu yoyote ambayo hataki. Mahakimu hao pia walisisitiza kwamba, “kuheshimu uamuzi wa mgonjwa wa kukubali au kukataa matibabu fulani ni mojawapo ya mambo ya msingi katika sekta ya afya.”

Tukiwa undugu wa ulimwenguni pote, tunafurahia uamuzi wa mahakama hiyo wa kuunga mkono haki ya Dada Pindo Mulla na ya mamilioni ya watu ya kuchagua matibabu watakayopata ikitegemea mambo wanayoamini.