DESEMBA 27, 2022
UJERUMANI
Mashahidi wa Yehova Nchini Ujerumani Wafungua Kesi Mpya Kuhusu Hifadhi ya Annemarie Kusserow
Uthibitisho Uliopatikana Hivi Karibuni Unaonyesha Kwamba Hifadhi ya Annemarie Inapaswa Kumilikiwa na Mashahidi wa Yehova
Kama ilivyotajwa awali kwenye jw.org na pia kwenye gazeti la The New York Times, wasimamizi wa Maonyesho ya Historia ya Kijeshi ya Bundeswehr yaliyo Dresden, Ujerumani, wamekataa kuwakabidhi Mashahidi wa Yehova hifadhi ya Dada Annemarie Kusserow. Kwa kufanya hivyo, wameenda kinyume na wosia wa dada huyo. Hata hivyo, uthibitisho uliopatikana hivi karibuni, unawaunga mkono Mashahidi wa Yehova. Kwa sababu hiyo, tengenezo letu limefungua kesi mpya dhidi ya usimamizi wa maonyesho hayo.
Kwa zaidi ya miaka saba, Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakijitahidi kufikia makubaliano kwa amani na wasimamizi wa maonyesho hayo bila mafanikio. Basi tengenezo letu likapeleka kesi mahakamani. Kwa kusikitisha, mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo mwaka wa 2021, kwa sababu ilikuwa na maoni ya kwamba usimamizi wa maonyesho hayo ulinunua hifadhi hiyo kwa kufuata sheria na kwa unyoofu.
Hazina ya Kihistoria
Annemarie alipokuwa na umri wa miaka 26, alianza kutengeneza hifadhi kwa kukusanya habari zilizohusu mambo ambayo Mashahidi wa Yehova walipitia katika kipindi cha Maangamizi. Aliitunza hifadhi hiyo kwa zaidi ya miaka 65, na wakati mwingine hata akihatarisha uhai wake ili kufanya hivyo, mpaka alipokufa katika mwaka wa 2005. Vitu ambavyo alihifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo, na hasa kwa ajili ya waabudu wenzake, vinaonwa kimataifa kuwa hazina ya kihistoria.
Annemarie alikusanya habari kwa ajili ya hifadhi hiyo kwa sababu alitaka watu wengi iwezekanavyo, Mashahidi wa Yehova na wengineo, waendelee kujifunza kutokana na historia ya uaminifu ya familia ya Kusserow. Ili kuhakikisha lengo hilo linafikiwa, alisema kwamba hifadhi hiyo itakuwa urithi wa jamii ya kidini ya Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, bado wosia wake haujatekelezwa.
Annemarie, pamoja na wadogo zake wanne, walihojiwa katika filamu ya Uingereza ya 1991 inayoitwa Purple Triangles. Filamu hiyo ilitumia mambo ambayo familia ya Kusserow ilipitia kueleza jinsi Mashahidi wa Yehova walivyoteswa kwa sababu ya kukataa kukana imani yao na kukataa kutoa kiapo cha uaminifu kwa Hitler. Filamu hiyo inamwonyesha Annemarie akiwa na hati mbalimbali na picha alizokusanya.
Muda mfupi kabla ya kifo chake, Annemarie alihojiwa na akaeleza kwamba pindi fulani askari wa Gestapo walimkamata nyumbani kwake na karibu apoteze baadhi ya vitu muhimu alivyokuwa amekusanya kwa ajili ya hifadhi hiyo. Alisema: “Nilikuwa nimeweka mkoba wangu karibu na mwingilio wa vyumba. Mkoba huo ulikuwa na barua na hati nyingine.” Alikuwa amejaza mkoba huo matofaa, akitazamia kwamba baada ya maofisa kuyaona, hawatachunguza kilicho chini yake. Alijiambia kwamba ikiwa mpango wake hautafaulu, ‘Angalau atakuwa na kitu cha kula gerezani.’ Inapendeza kwamba mpango wake ulifaulu.
Yauzwa Kinyume na Sheria
Muda mfupi baada ya Annemarie kufa, hifadhi hiyo ilitoweka. Ilikuja kugunduliwa kwamba mmoja wa kaka za Annemarie ambaye alikuwa ameacha kushirikiana na Mashahidi wa Yehova alichukua hifadhi hiyo kutoka nyumbani kwa Annemarie na kuiuza kwa usimamizi wa jumba la maonyesho. Kaka huyo alishakufa.
Washiriki waliobaki wa familia ya Kusserow, walijua vizuri wosia wa Annemarie na walishangaa sana mahakama ilipoamua kwamba usimamizi wa maonyesho utabaki na hifadhi hiyo. Kuanzia wakati huo, familia, marafiki, na Mashahidi wengine wa Yehova ambao waliteswa na Wanazi, wametuma mamia ya barua kwenye maonyesho hayo, na kwenye Wizara ya Ulinzi ambayo inasimamia maonyesho hayo, wakiwasihi warudishe hifadhi hiyo kwa Mashahidi wa Yehova kama alivyotaka Annemarie.
Vitu vya Pekee
Baadhi ya vitu muhimu vilivyo kwenye hifadhi hiyo ni barua aliyoandika Wilhelm, kaka ya Annemarie, ili kuaga familia yao, aliiandika, Aprili 26, 1940. Wilhelm alikataa kujiunga na jeshi kwa sababu alikuwa Shahidi wa Yehova na dhamiri yake haikumruhusu. Kwa hiyo, Wanazi walimpa hukumu ya kifo.
Barua ya Wilhelm inasema: “Wazazi wangu wapendwa, kaka zangu na dada zangu: Nyote mnajua kwamba ninawapenda sana, na kila mara ninapotazama picha ya familia yetu, ninahisi hivyo. Sikuzote tulikuwa na umoja na maisha mazuri nyumbani. Hata hivyo, zaidi ya yote ni lazima tumpende Mungu, kama kiongozi wetu Yesu Kristo alivyotuagiza. Tukiwa washikamanifu kwake, atatuthawabisha.” Aliuawa kwa kupigwa risasi asubuhi ya Aprili 27 akiwa na umri wa miaka 25.
Franz na Hilda Kusserow, wazazi wa Annemarie, walikuwa na watoto 11. Kama ilivyokuwa kwa Wilhelm, Franz na vijana wake wengine wa kiume walitupwa gerezani kwa sababu ya kukataa kushiriki katika vita. Watoto ambao walikuwa wadogo zaidi walikataa kutoa salamu ya kumsifu Hitler na hivyo wakatenganishwa na wazazi wao na kupelekwa kwenye shule za kurekebisha tabia na baadaye wakapelekwa kulelewa na familia nyingine.
Wolfgang, mmoja wa vijana wa Kusserow alipopelekwa mbele ya mahakama ya kijeshi, alisema hivi kwa ujasiri: “Nililelewa na Mashahidi wa Yehova, nao waliishi kupatana na neno la Mungu lililoandikwa katika Maandiko Matakatifu. Sheria kuu na takatifu zaidi aliyowapa wanadamu ni: ‘Mpende Mungu wako kuliko kitu kingine chochote na jirani yako kama wewe mwenyewe.’ Sheria nyingine inasema hivi: ‘Usiue.’ Je, Muumba wetu aliiandikia miti maneno hayo yote?”
Machi 28, 1942, Wolfgang aliuawa kwa kukatwa kichwa akiwa na umri wa miaka 20.
Suala la Imani
Annemarie na familia yao waliteseka sana kwa sababu ya imani yao na msimamo wao thabiti wa kutounga mkono jeshi la Wanazi katika vita, na hata baadhi ya washiriki wa familia hiyo waliuawa kwa sababu walikataa kuua watu. Kwa ujumla, familia yote ilifungwa gerezani kwa zaidi ya miaka 47.
Hifadhi hiyo inatusaidia kuelewa vizuri imani ya pekee ambayo ilionyeshwa na familia hiyo. Mambo yaliyo kwenye hifadhi hiyo yanaonyesha jinsi imani inavyoweza kumpa mtu nguvu hata anapokabili mateso makali na hata kutishiwa kuuawa. Masomo hayo muhimu ambayo tunapata kutokana na hifadhi hiyo yataeleweka na kuthaminiwa hata zaidi yakiwekwa katika maonyesho ya Mashahidi wa Yehova.
Paul Gerhard Kusserow, mwana wa mwisho wa familia ya Kusserow ambaye alikuwa hai, alikufa mwezi wa Oktoba 2022. Alitazamia kwa hamu siku ambayo jumba la maonyesho ya kijeshi lingetekeleza wosia wa dada yake na alitetea kutekelezwa kwa jambo hilo hadharani hadi alipokufa. Alikuwa akisema: “Kaka zangu walikufa kwa sababu walikataa kujiunga na jeshi. Kwa kweli, ninaamini kwamba haifai kabisa kuweka hifadhi hii katika jumba la maonyesho ya kijeshi.”
Mashahidi wa Yehova wanakubaliana naye. Ni ukosefu mkubwa wa haki kwa wasimamizi wa maonyesho hayo kupuuza maelezo ya wazi ya Annemarie. Haki za familia ya Kusserow zilikiukwa katika kipindi cha Ujamaa wa Kitaifa na bado zinakiukwa tena katika Ujerumani ya sasa.
Inasikitisha kwamba hifadhi yenyewe pia haijaheshimiwa. Kati ya vitu zaidi ya 1,000 ni vitu 6 tu ambavyo vinaonyeshwa kwenye maonyesho hayo, vingine vyote vimewekwa kwenye chumba cha kuhifadhia vitu na watu hawawezi kuviona na kunufaika.
Tunasali kwamba hatimaye mahakama itawapa Mashahidi wa Yehova hifadhi hiyo kwa sababu wana haki ya kisheria na kimaadili ya kuimiliki.—Luka 18:7.