Hamia kwenye habari

Blue Planet Archive/Mark Conlin

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Jinsi Samaki Anayeitwa Grunion Anavyotaga Mayai Yake

Jinsi Samaki Anayeitwa Grunion Anavyotaga Mayai Yake

 Kuna samaki mdogo anayeitwa grunion wa California. Samaki huyu hutaga mayai yake kwenye ufuo wa California nchini Marekani na kwenye ufuo wa Baja California nchini Mexico. Samaki hawa wanajua siku na muda hususa wanaopaswa kutaga mayai ili mayai yao yafaulu kuanguliwa na kutokeza kizazi kinachofuata.

 Fikiria hili: Kwa sababu ya mwezi mpevu au mwezi mpya kunakuwa na mawimbi makubwa sana na bahari inajaa kabisa. Siku tatu au nne baadaye, bahari inakuwa imerudi na katika kipindi hicho samaki hao wanataga mayai yao. Ikiwa wangetaga mayai yao kabla ya mwezi mpevu au mwezi mpya kutokea basi mayai yao yangebebwa na mawimbi makubwa yanayochukua mchanga ufuoni. Hata hivyo, kwa sababu wanataga mayai baada ya bahari kurudi, mawimbi yanakuwa ni madogo na yanaleta mchanga kutoka baharini na hivyo mayai hayo yanafunikwa vizuri.

Wally Skalij/Los Angeles Times via Getty Images

 Jambo lingine ni kwamba wao hutaga mayai yao katika majira ya kuchipua na majira ya kiangazi. Katika majira hayo mawimbi ni makubwa zaidi usiku kuliko mchana na kwa kuwa samaki hao hutaga mayai usiku, mawimbi yanawawezesha kufika mbali zaidi ufuoni ili kutaga mayai yao katika sehemu ambayo mawimbi mengine yatakayokuja hayatafika.

 Samaki hao husubiri wimbi kubwa ambalo litawabeba hadi ufuoni. Wanapofika ufuoni, wao hujiburuta kwenye mchanga ili wafike mbali kadiri wawezavyo. Samaki jike hudidimiza mwili wake kwenye mchanga wenye unyevunyevu akianza na mkia wake. Kwa hiyo, nusu ya mwili wake inakuwa imefunikwa na mchanga kisha anataga mayai yake humo na yanakuwa sentimita tano hadi nane ndani ya mchanga. Samaki jike anapoendelea kutaga mayai naye samaki dume anaweka mbegu za kiume. Wanapomaliza, samaki hao hujiburuta wakielekea kwenye maji ili wabebwe na wimbi lingine litakalowarudisha baharini.

 Mayai yakiwa ndani ya mchanga huo wenye unyevunyevu yanaendelea kukua lakini pia yanahitaji kutikiswa-tikiswa na mawimbi ya bahari ili yaanguliwe. Baada ya majuma mawili kunakuwa na mawimbi makubwa kabisa na hivyo samaki wadogo wanaanguliwa. Hata hivyo, ikiwa mawimbi si makubwa, mayai hayo yanaweza kubaki ndani ya mchanga kwa majuma mengine manne yakisubiri mawimbi makubwa ili yaweze kuanguliwa.

 Una maoni gani: Je, uwezo wa samaki anayeitwa grunion wa kujua muda hususa wa kutaga mayai na jinsi ya kufika mahali pa kuyatagia umejitokeza wenyewe? Au, je, umebuniwa?