JE, NI KAZI YA UBUNI?
Uwezo wa Kujisafisha wa Ngozi ya Nyangumi Anayeitwa Pilot
Viumbe wa baharini wanaokua kwenye sehemu za nje za meli huwatatiza sana watu wanaoendesha meli. Viumbe hao hupunguza kasi ya meli, hufanya zitumie mafuta mengi zaidi kuendeshwa, na kuzuia zisifanye kazi kwa muda fulani baada ya miaka kadhaa ili zisafishwe. Wanasayansi wanageukia vitu vya asili kupata suluhisho.
Jambo la kufikiria: Uchunguzi umeonyesha kwamba ngozi ya nyangumi anayeitwa pilot mwenye pezi refu (Globicephala melas) ina uwezo wa kujisafisha. Ina mianya midogo sana, ambayo hairuhusu viumbe wa baharini kujishikilia. Nafasi iliyo katikati ya mianya hiyo imejaa umajimaji fulani unaoshambulia miani na bakteria. Kila mara nyangumi anapovua ngozi yake, anatokeza umajimaji mpya.
Wanasayansi wanapanga kutumia mfumo huo wa nyangumi wa kujisafisha kwenye sehemu ya nje ya meli. Zamani, rangi zinazozuia viumbe wa baharini kujishikiza zilikuwa zinatumiwa. Hata hivyo, hivi karibuni mojawapo ya rangi zilizotumiwa sana imepigwa marufuku kwa sababu inaua wanyama wa baharini. Suluhisho la watafiti ni kufunika sehemu ya nje ya meli kwa wavu uliotengenezwa kwa nyaya juu ya mashimo yanayotoa kemikali isiyodhuru mazingira. Kemikali hiyo huongezeka uzito inapogusa maji ya bahari, na kufanyiza ngozi inayofunika sehemu yote ya mbele. Baada ya muda, ngozi hiyo yenye upana wa milimita 0.7 hivi, huisha na kuondolewa pamoja na viumbe wowote waliokuwa wamejishikiza hapo. Kisha mfumo huo hutokeza umajimaji mwingine wa kufunika sehemu hiyo ya mbele.
Majaribio yaliyofanywa katika maabara yameonyesha kwamba mfumo huo unaweza kusuluhisha kabisa tatizo hilo linaloathiri meli. Hiyo itakuwa faida kubwa kwa kampuni za usafirishaji kwa sababu kutoa meli baharini ili tu isafishwe kunagharimu sana.
Una maoni gani? Je, uwezo wa kujisafisha wa ngozi ya nyangumi huyu ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?