JE, NI KAZI YA UBUNI?
Shingo ya Chungu
MAINJINIA wanastaajabishwa na uwezo wa chungu wa kawaida kuinua vitu vizito kuliko mwili wake. Ili kuelewa uwezo huo, mainjinia wa Chuo Kikuu cha Ohio huko Marekani walitumia kompyuta kutengeneza kifaa kinachoiga jinsi mwili ya chungu unavyofanya kazi. Walitengeneza kifaa hicho kwa kutegemea picha za eksirei zilizoonyesha kwa ndani mwili wa chungu na nguvu anazotumia anapobeba mizigo.
Sehemu muhimu katika mwili wa chungu ni shingo, ambayo huitumia kuinua vitu vizito anavyobeba kwa mdomo wake. Tishu laini zilizo katika shingo yake huunganisha mwili na kichwa. Mtafiti mmoja alisema hivi: “Muundo wa muungano wa tishu laini na sehemu ngumu ya mwili ni muhimu ili shingo yake ifanye kazi vizuri. Muungano huo wa pekee kati ya viungo laini na vigumu huenda ndio unaofanya shingo yake kuwa imara na kumwezesha ainue vitu vyenye uzito mkubwa.” Watafiti wanaamini kwamba kuelewa vizuri jinsi ambavyo shingo ya chungu hufanya kazi kutachangia kuunda roboti za kisasa.
Una Maoni Gani? Je, shingo ya chungu iliyounganishwa kwa njia tata ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?