Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mgogoro Kati ya Galileo na Kanisa

Mgogoro Kati ya Galileo na Kanisa

Mgogoro Kati ya Galileo na Kanisa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

LEO ni Juni 22, 1633. Mzee mmoja dhaifu amepiga magoti mbele ya Mahakama ya Kuhukumu Waasi ya Roma. Yeye ni mmojawapo wa wanasayansi maarufu wa wakati huu. Dhana zake za kisayansi zinategemea uchunguzi na utafiti ambao amefanya kwa miaka mingi. Hata hivyo, iwapo anataka kuokoa uhai wake, itambidi akane mambo anayojua ni ya kweli.

Mzee huyo aliitwa Galileo Galilei. Kesi hiyo inayojulikana na wengi kuwa kesi ya Galileo, imezusha mashaka, maswali, na mabishano ambayo yamedumu hadi leo, miaka 370 hivi baadaye. Kesi hiyo imeathiri sana historia ya dini na sayansi. Kwa nini kesi hiyo imeleta ubishi mwingi? Kwa nini vyombo vya habari vimezungumzia kesi ya Galileo katika siku zetu? Je, inaonyesha kwamba “sayansi na dini hazipatani,” kama mwandishi mmoja anavyosema?

Galileo huonwa na wengi kuwa “mwanzilishi wa sayansi ya kisasa.” Alikuwa mtaalamu wa hesabu na wa anga na vilevile mwanafizikia. Akiwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kuchunguza anga kwa kutumia darubini, Galileo alitumia mambo aliyoona kuunga mkono dhana iliyoleta ubishi mkubwa nyakati hizo: Kwamba dunia huzunguka jua na hivyo sayari yetu haiko katikati ya ulimwengu. Si ajabu kwamba Galileo huonwa kuwa mwanzilishi wa njia ya kisasa ya kufanya utafiti ili kuthibitisha nadharia fulani!

Ni yapi yaliyokuwa baadhi ya mavumbuzi ya Galileo? Akiwa mtaalamu wa mambo ya angani, alivumbua kwamba sayari ya Sumbula huzungukwa na miezi, kwamba Kilimia ni mkusanyo wa nyota, kwamba mwezi una milima, na kwamba sayari ya Zuhura huonekana ikibadilika kulingana na mzunguko wake sawa na vile mwezi unavyobadilika. Akiwa mwanafizikia, alichunguza sheria zinazohusu mizani ya saa na jinsi vitu vinavyoanguka. Galileo alivumbua vifaa kama vile bikari, yaani, chombo cha kuchorea duara ambacho hutumiwa katika hesabu. Akitumia habari alizopokea kutoka Uholanzi, aliunda darubini ambayo ilimsaidia kuchunguza anga.

Hata hivyo, mgogoro kati yake na mamlaka ya kanisa ulifanya kazi ya mwanasayansi huyo maarufu izushe ubishi ulioendelea kwa muda mrefu. Mgogoro huo ulianzaje, na ulisababishwa na nini?

Mabishano na Kanisa Katoliki

Galileo alianza kuamini nadharia ya Copernican mwishoni mwa karne ya 16. Nadharia hiyo inasema kwamba dunia huzunguka jua, na si jua kuzunguka dunia. Alipotumia darubini yake mnamo mwaka wa 1610 kuvumbua magimba ya angani ambayo hayakuwa yamewahi kuonekana, Galileo alisadiki kuwa amethibitisha ukweli wa nadharia ya Copernican.

Kulingana na kitabu Grande Dizionario Enciclopedico UTET, Galileo alitaka kufanya mengi zaidi ya kuvumbua mambo hayo. Alitaka kuwasadikisha “watu wa ngazi za juu zaidi wa wakati huo (wakuu na makadinali)” kwamba nadharia ya Copernican ilikuwa ya kweli. Alitumaini kwamba kwa msaada wa marafiki mashuhuri, angeshinda vizuizi vilivyowekwa na kanisa na hata kuungwa mkono nalo.

Mnamo mwaka wa 1611, Galileo alisafiri hadi Roma, ambapo alikutana na viongozi wakuu wa kanisa. Alitumia darubini yake kuwaonyesha mambo ambayo alikuwa amevumbua kuhusu anga. Lakini mambo hayakuenda kama alivyotarajia. Kufikia mwaka wa 1616, Galileo alijikuta akichunguzwa na Kanisa.

Wanatheolojia wa Mahakama ya Kuhukumu Waasi ya Roma walisema kwamba nadharia ya Copernican “ilikuwa ya kipumbavu, ya kipuuzi na ya uasi, kwa sababu ilipingana kwa njia nyingi na maana ya neno kwa neno ya vifungu fulani vya Maandiko Matakatifu, jinsi wengi wanavyoyaelewa, na maoni ya Mababa Watakatifu na wanatheolojia maarufu.”

Galileo alikutana na kadinali Robert Bellarmine aliyeonwa kuwa mwanatheolojia maarufu zaidi wa Kikatoliki wa wakati huo na aliyekuwa “kiboko cha waasi.” Bellarmine alimwonya Galileo kirasmi akome kuendeleza maoni yake kwamba dunia haiko katikati ya ulimwengu.

Afikishwa Mbele ya Mahakama ya Kuhukumu Waasi

Galileo alijaribu kutumia busara, lakini hakuacha kuitetea nadharia ya Copernican. Miaka 17 baadaye, mnamo mwaka wa 1633, Galileo alifikishwa mbele ya Mahakama ya Kuhukumu Waasi. Kadinali Bellarmine alikuwa amekufa na sasa mshtaki wake mkuu alikuwa Papa Urban wa Nane, ambaye hakumpinga hapo awali. Waandishi wameona hiyo kuwa kesi maarufu sana na isiyo ya haki katika historia, hata wamesema ni maarufu kama ile ya Socrates na ya Yesu.

Kesi hiyo ilianzaje? Galileo aliandika kitabu kiitwacho Dialogue Concerning the Two Chief World Systems ambacho kiliunga mkono nadharia ya Copernican. Mwandishi huyo aliagizwa afike kwenye mahakama hiyo mnamo mwaka wa 1632, lakini alikawia kwa kuwa alikuwa mgonjwa na umri wake ulikuwa karibu miaka 70. Mwaka uliofuata, alisafiri hadi Roma baada ya kutishwa kwamba angefungwa na kusafirishwa kwa nguvu. Kwa amri ya papa, alihojiwa na hata kutishwa kwamba angeteswa.

Haijulikani kama mzee huyo aliteswa. Kama rekodi ya hukumu yake inavyosema, Galileo “alihojiwa vikali.” Italo Mereu, mtaalamu wa historia ya sheria ya Italia, anasema kwamba nyakati hizo usemi huo ulitumiwa kuelezea mateso. Wasomi kadhaa wanaunga mkono maelezo hayo.

Kwa vyovyote vile, Galileo alihukumiwa mnamo Juni 22, 1633, katika jumba lenye umati uliokuwa kimya mbele ya Mahakama ya Kuhukumu Waasi. Alipatikana na hatia ya “kushikilia na kuamini fundisho la uwongo, kinyume na Maandiko Matakatifu ya Mungu, kwamba Jua . . . halisongi kutoka mashariki hadi magharibi, bali Dunia ndiyo husonga nayo haiko katikati ya ulimwengu.”

Galileo hakutaka kufa kwa ajili ya mambo aliyoamini, hivyo alilazimika kuikana imani yake. Hukumu yake iliposomwa, mwanasayansi huyo mzee aliyekuwa amepiga magoti na kuvalia mavazi ya toba, alitamka maneno haya kwa huzuni: “Ninakana, ninalaani, na ninachukia makosa yaliyotajwa na maasi [yaani, nadharia ya Copernican] na makosa yote kwa ujumla, uasi, au kikundi chochote kinachopinga Kanisa Takatifu.”

Kulingana na hekaya moja maarufu ambayo haijathibitishwa kabisa, Galileo alipokana uvumbuzi wake, aligongesha mguu wake chini kwa kishindo na akateta akisema hivi: “Na bado inasonga!” Waelezaji fulani husema kwamba mwanasayansi huyo aliaibika sana kutokana na tukio hilo la kukana yale aliyoamini, hivyo akapatwa na hisia za majuto hadi kifo chake. Alihukumiwa kifungo cha gerezani, lakini hukumu hiyo ilibadilishwa na kuwa kifungo cha maisha akiwa amezuiliwa nyumbani. Pole kwa pole alianza kupofuka, hivyo akaishi maisha ya upweke.

Je, Ulikuwa Mgogoro Kati ya Dini na Sayansi?

Watu wengi wamekata kauli kwamba kesi ya Galileo ilionyesha kwamba sayansi na dini haziwezi kupatana kwa vyovyote. Hivyo, kesi hiyo imefanya watu waikimbie dini. Kesi hiyo imewasadikisha wengi kwamba dini ni tisho kwa maendeleo ya kisayansi. Je, hiyo ni kweli?

Ni kweli kwamba Papa Urban wa Nane na wanatheolojia wa Mahakama ya Kuhukumu Waasi waliipinga nadharia ya Copernican, wakidai eti ilipingana na Biblia. Washtaki wa Galileo walitumia maneno ya Yoshua yanayosema, “Wewe Jua, simama kimya,” ambayo kulingana nao, yalipaswa kueleweka jinsi yalivyo. (Yoshua 10:12) Lakini, je, kweli Biblia inapingana na nadharia ya Copernican? La hasha.

Tofauti hiyo kati ya sayansi na Biblia ilitokana na kuyaeleza Maandiko kwa njia ambayo kwa kweli si sahihi. Hayo ndiyo yaliyokuwa maoni ya Galileo. Alimwandikia hivi mwanafunzi wake: “Ijapokuwa Maandiko hayawezi kukosea, wafasiri na waelezaji wanaweza kukosea kwa njia nyingi. Mara nyingi wao hukosea sana wanapofasiri Maandiko neno kwa neno.” Mwanafunzi yeyote wa Biblia aliye makini atakubali jambo hilo. *

Galileo hakukomea hapo. Alidai kwamba kwa kuwa vitabu viwili, yaani Biblia na kitabu cha asili, viliandikwa na Mtungaji mmoja, basi haviwezi kupingana. Hata hivyo, aliongeza kusema kuwa haiwezekani “kuwa na uhakika kwamba wafasiri wote huongozwa na Mungu.” Huenda uchambuzi huo usio wa moja kwa moja wa maelezo rasmi ya kanisa ulionwa kuwa uchokozi, na hivyo ukasababisha mwanasayansi huyo ahukumiwe na Mahakama ya Kuhukumu Waasi ya Roma. Kwa maoni yao, mtu asiyefahamu lolote kuhusiana na mambo ya dini hakupaswa kuthubutu kukosoa mamlaka ya kanisa.

Kuhusu kesi ya Galileo, wasomi fulani wameshuku ukweli wa dai la kwamba kanisa na papa hawawezi kukosea. Mwanatheolojia Mkatoliki Hans Küng aliandika kwamba “mafundisho ya kanisa” kutia ndani “hukumu ya Galileo” ni makosa “mengi na ya wazi” ambayo yanaonyesha kwamba kanisa na papa wanaweza kukosea.

Je, Galileo Ameondolewa Lawama?

Mnamo Novemba 1979, mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa, John Paul wa Pili alitaka kesi ya Galileo ichunguzwe upya, kwani papa huyo alikubali kwamba Galileo “aliteseka sana . . . mikononi mwa Kanisa.” Mnamo mwaka wa 1992, miaka 13 baadaye, tume iliyoteuliwa na papa huyo ilikiri hivi: “Wanatheolojia fulani, walioishi wakati wa Galileo, . . . walishindwa kuelewa maana ya kindani ya Maandiko yanayofafanua muundo wa ulimwengu.”

Ukweli ni kwamba si wanatheolojia tu walioikosoa nadharia ya Copernican. Papa Urban wa Nane, aliyetimiza daraka muhimu katika kesi hiyo, alisisitiza vikali kwamba Galileo alipaswa kuacha kudhoofisha fundisho la muda mrefu la kanisa linalosema kwamba dunia iko katikati ya ulimwengu. Fundisho hilo lilitokana na mwanafalsafa Mgiriki Aristotle, wala si katika Biblia.

Tume hiyo ya kisasa ilipochunguza tena kesi ya Galileo kwa undani, papa alisema kwamba uamuzi uliotolewa ulikuwa “wa haraka na usiofaa.” Je, mwanasayansi huyo alikuwa akiondolewa lawama? Mwandishi mmoja anasema hivi: “Ni upuuzi kusema kwamba Galileo alikuwa akiondolewa lawamani kama wengine wanavyosema, kwa sababu historia inahukumu mahakama hiyo ya kanisa wala si Galileo.” Mwanahistoria Luigi Firpo alisema: “Wanyanyasaji hawana haki ya kuwaondolea lawama watu ambao waliwanyanyasa.”

Biblia ni “taa yenye kung’aa mahali penye giza.” (2 Petro 1:19) Galileo aliitetea Biblia dhidi ya kufasiriwa kimakosa. Lakini kanisa lilifanya kinyume chake, kwa kutetea desturi zilizotungwa na wanadamu za tangu zamani bila kuijali Biblia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 24 Msomaji yeyote mwenye kufuata haki atakubali kwamba kusema jua limesimama angani kunamaanisha kwamba hivyo ndivyo mtu anavyoliona, wala si mchanganuo wa kisayansi. Hata wataalamu wa mambo ya angani mara nyingi husema kwamba jua, sayari, na nyota huchomoza na kutua. Huwa hawamaanishi kwamba magimba hayo ya mbinguni huzunguka dunia, lakini, badala yake, hayo huonekana kana kwamba yanasonga angani.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]

Maisha ya Galileo

Galileo alizaliwa huko Pisa mnamo mwaka wa 1564 na alisomea tiba kwenye chuo kikuu cha huko. Babake alikuwa mzaliwa wa Florence. Galileo hakupenda somo hilo, hivyo aliliacha na kuanza kusomea fizikia na hesabu. Mnamo mwaka 1585, alirejea nyumbani kwao bila cheti chochote cha masomo. Hata hivyo, alikuwa ameheshimiwa na wataalamu wakuu zaidi wa hesabu wa nyakati hizo, na alipewa cheo cha mhadhiri wa hesabu katika Chuo Kikuu cha Pisa. Baada ya kifo cha babake, matatizo ya kifedha yalimlazimu Galileo ahamie Padua, ambako alipewa cheo chenye mshahara mnono zaidi cha msimamizi wa idara ya hesabu katika chuo kikuu cha jiji hilo.

Katika muda wa miaka 18 ambayo aliishi Padua, mwanamke mchanga Mvenetia alimzalia watoto watatu. Mnamo mwaka wa 1610, alirudi Florence ambako hali zilimruhusu atumie wakati mwingi zaidi kufanya utafiti. Hata hivyo, hakupata uhuru mwingi kama aliopata alipokuwa akiishi katika eneo la Jamhuri ya Venetia. Mtawala wa Tuscany alimteua kuwa “mwanafalsafa na mtaalamu wa hesabu wa kwanza.” Galileo alikufa huko Florence katika mwaka wa 1642 alipokuwa anatumikia kifungo cha nyumbani alichohukumiwa na Mahakama ya Kuhukumu Waasi.

[Hisani]

From the book The Library of Original Sources, Volume VI, 1915

[Picha katika ukurasa wa 12]

Darubini ya Galileo, ambayo ilimsaidia kuthibitisha kwamba dunia haiko katikati ya ulimwengu

[Hisani]

Scala/Art Resource, NY

[Picha katika ukurasa wa 12]

Mfumo unaoonyesha kwamba dunia iko katikati ya ulimwengu

Mfumo unaoonyesha kwamba jua liko katikati ya ulimwengu

[Hisani]

Background: © 1998 Visual Language

[Picha katika ukurasa wa 11]

Picture: From the book The Historian’s History of the World