Kwa Nini Watu Wengi Zaidi Wanasherehekea Krismasi?
Kwa Nini Watu Wengi Zaidi Wanasherehekea Krismasi?
JE, WEWE hutazamia Krismasi kwa hamu? Au wewe hujawa na wasiwasi wakati huo unapokaribia? Mamilioni ya watu hujiuliza: ‘Nitamnunulia nani zawadi? Ninunue zawadi gani? Je, nina pesa za kutosha kuinunua? Nikikopa, itanichukua muda gani kulipa deni langu?’
Hata ingawa watu huwa na mahangaiko hayo, bado Krismasi ni sherehe inayopendwa sana. Kwa kweli, sherehe hiyo imeenea kufikia nchi ambazo si za Kikristo. Huko Japani, familia nyingi husherehekea Krismasi, si kwa sababu za kidini, lakini kwa sababu ni pindi ya sherehe. Huko China “madirisha ya maduka mengi katika majiji makubwa huwa na picha ya Baba Krismasi,” linasema jarida The Wall Street Journal, na linaongezea hivi: “Roho ya Krismasi imeanza kuwanasa watu wanaoishi katika miji ya China nao wanaona hiyo kuwa nafasi ya kununua vitu, kula na kuwa na karamu.”
Kusherehekea Krismasi kumeinua sana uchumi wa nchi nyingi ulimwenguni. Imekuwa hivyo hasa kwa China, ambayo sasa “inasafirisha kwa wingi sana miti ya plastiki, mapambo, taa zinazomweka-mweka, na mapambo mengine ya Krismasi,” linasema jarida The Wall Street Journal.
Pia nchi za Kiislamu zinaendeleza sherehe zinazofanana na zile za Krismasi, ingawa huenda zisifanywe Desemba (Mwezi wa 12) 25. Huko Ankara, Uturuki, na Beirut, Lebanoni, si ajabu kuona madirisha ya maduka yakiwa na miti iliyofunikwa mapambo na zawadi zilizopakiwa katika karatasi za pekee. Nchini Indonesia, hoteli na maduka makubwa huandaa sherehe ambapo watoto wanaweza kula pamoja na Baba Krismasi au wapigwe picha pamoja naye.
Katika nchi nyingi za Kikristo, Krismasi ni wakati hasa wa biashara, na matangazo mengi ya kibiashara “yamekusudiwa hasa ili kuwanasa watoto,” linasema jarida Royal Bank Letter la Kanada. Kwa kweli, bado watu fulani huenda kanisani ili kuadhimisha Krismasi. Lakini nyimbo za Krismasi husikika hasa katika maduka makubwa, kwani siku hizi hayo ndiyo yamekuwa mahekalu. Kwa nini kumekuwa na badiliko hilo? Je, huenda ikawa ni kwa sababu ya chanzo cha Krismasi? Krismasi ilianzia wapi?
Kabla ya kuzungumzia maswali hayo, ingefaa tusome masimulizi ya Biblia ambayo hutumiwa kuigiza Mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
WAANDIKAJI WA INJILI WANASEMA NINI?
Mtume Mathayo: “Baada ya Yesu kuzaliwa katika Bethlehemu ya Yudea siku za Mfalme Herode, tazama! wanajimu kutoka sehemu za mashariki walikuja Yerusalemu, wakisema: ‘Yuko wapi yule mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa? Kwa maana tuliiona nyota yake wakati tulipokuwa mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.’ Aliposikia hilo Mfalme Herode akafadhaika.” Kwa hiyo, Herode akawauliza “wakuu wa makuhani . . . ni wapi Kristo alipaswa kuzaliwa.” Alipoambiwa kwamba angezaliwa “katika Bethlehemu,” Herode akawaambia hivi wale wanajimu: “Nendeni mkamtafute kwa uangalifu yule mtoto mchanga, na mkiisha kumpata nileteeni habari.”
“Waliondoka wakaenda; na, tazama! nyota waliyokuwa wameona wakati walipokuwa mashariki ikaenda mbele yao, mpaka ikaja kutua juu ya mahali alipokuwa yule mtoto mchanga. . . . Walipoingia ndani ya ile nyumba wakamwona huyo mtoto mchanga pamoja na Maria mama yake.” Baada ya kumpa Yesu zawadi hizo, “walipewa onyo la kimungu katika ndoto wasirudi kwa Herode, [kwa hiyo] wakaondoka kwenda nchi yao kwa njia nyingine.”
“Walipokuwa wamekwisha kuondoka, tazama! malaika wa Yehova akamtokea Yosefu katika ndoto, akisema: ‘Simama, mchukue huyo mtoto mchanga na mama yake mkimbie kuingia Misri . . .’ Kwa hiyo akasimama na kuchukua pamoja naye mtoto huyo mchanga na mama yake wakati wa usiku, akaondoka . . . Ndipo Herode, alipoona ameshindwa akili na wale wanajimu, akaingiwa na ghadhabu kubwa, akatuma watu na kuagiza wavulana wote katika Bethlehemu na katika wilaya zake zote wauawe, kuanzia umri wa miaka miwili kwenda chini.”—Mathayo 2:1-16.
Mwanafunzi Luka: Yosefu “akapanda kutoka Galilaya, kutoka jiji la Nazareti, akaingia Yudea, kwenye jiji la Daudi, linaloitwa Bethlehemu, . . . ili apate kuandikishwa pamoja na Maria . . . Walipokuwa huko, . . . akamzaa mwana wake, mzaliwa wa kwanza, akamfunga vitambaa na kumlaza katika hori, kwa sababu hapakuwa na mahali kwa ajili yao katika chumba cha kukaa.”
“Katika nchi hiyo kulikuwako pia wachungaji wakiishi nje, wakichunga makundi yao usiku. Na kwa ghafula malaika wa Yehova akasimama kando yao, . . . nao wakaogopa sana. Lakini malaika akawaambia: ‘Msiogope, kwa maana, tazama! ninawatangazia ninyi habari njema ya shangwe kubwa ambayo watu wote watakuwa nayo, kwa sababu leo katika jiji la Daudi, Mwokozi ambaye ni Kristo Bwana, amezaliwa kwenu.’” Wachungaji hao “wakaenda haraka wakamkuta Maria na vilevile Yosefu, na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori.”—Luka 2:4-16.