JE, NI KAZI YA UBUNI?
Ngozi ya Nyoka
KWA KUWA nyoka hawana miguu wala mikono, wanahitaji ngozi imara ili kuhimili msuguano ambao hutokea kila wanaposonga. Kuna aina za nyoka ambao hupanda kwenye miti inayokwaruza na wengine huchimba kwenye mchanga unaochubua. Ni nini kinachofanya ngozi ya nyoka istahimili hali hizo?
Fikiria hili: Unene na muundo wa ngozi ya nyoka hutofautiana kulingana na jamii za nyoka. Hata hivyo, ngozi za nyoka hufanana kwa njia hii: Ni ngumu upande wa nje bali huzidi kuwa laini kuelekea ndani ya mwili wa nyoka. Kwa nini hilo ni muhimu? Mtafiti anayeitwa Marie-Christin Klein anasema: “Vitu ambavyo ni vigumu upande wa nje na kuwa laini hatua kwa hatua upande wa ndani, vinaweza kutawanya shinikizo kwenye eneo kubwa zaidi.” Muundo wa kipekee wa ngozi ya nyoka huruhusu mvutano wa kutosha kati ya mwili na ardhi na hivyo kumfanya nyoka aweze kusonga, na wakati huohuo, kutawanya shinikizo lolote la mawe yaliyochongoka ili kupunguza uharibifu kwenye ngozi yake. Uimara wa ngozi ya nyoka ni muhimu, kwani wao huvua ngozi zao kila baada ya miezi miwili au mitatu.
Vifaa vinavyofanana na ngozi ya nyoka vinaweza kutumiwa kwa ajili ya matibabu—kwa mfano, katika kutengeneza viungo bandia visivyoteleza na vinavyodumu zaidi. Pia, mikanda ya kuendesha na kusukuma mashine ikitengenezwa kwa kuiga muundo wa ngozi ya nyoka, haitahitaji kutiwa grisi nyingi zenye kemikali zinazoharibu mazingira.
Una maoni gani? Je, ngozi ya nyoka ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?