NCHI NA WATU
Kutembelea Mongolia
GENGHIS KHAN, shujaa jasiri aliyeishi katika karne ya 12, aliweka msingi wa ile iliyokuja kuwa Milki kubwa ya Mongolia. Ikiwa sehemu ndogo ya eneo la milki hiyo, leo Mongolia imezungukwa na nchi ya Urusi na China na ni mojawapo ya nchi yenye watu wachache zaidi duniani.
Eneo la Mongolia linatia ndani maeneo makubwa yenye nyika za nyasi katika miinuko na mabonde, milima mirefu, mito, na vijito vya maji. Jangwa la Gobi linalojulikana kwa kuwa na mabaki ya dinosa, liko upande wa kusini mwa nchi hiyo. Nchi ya Mongolia iko mita 1,580 juu ya usawa wa bahari, na wenyeji huiita “Nchi Yenye Anga la Bluu.” Jina hilo linafaa, kwa kuwa Mongolia ina zaidi ya siku 250 katika mwaka ambazo hupata nuru ya jua!
Hali ya hewa katika Mongolia ni mbaya. Wakati wa kiangazi, kiwango cha joto kinaweza kufikia nyuzi 40 Selsiasi, na kipindi cha baridi, kiwango hicho hushuka
mpaka kufikia nyuzi 40 Selsiasi chini ya sifuri. Asilimia 33 hivi ya Wamongolia wanaishi maisha ya uhamaji. Wanaume na wanawake huanza siku asubuhi na mapema kwa kukamua maziwa ya mbuzi, ng’ombe, ngamia, na farasi. Kwa kawaida chakula cha Wamongolia hutia ndani vyakula vinavyotokana na maziwa na nyama, na wanapendelea kula nyama ya kondoo.Wamongolia ni wakarimu. Huhakikisha kwamba ger, au nyumba zao zilizo kama hema inayohamishika haifungwi mlango ili mgeni yeyote atakayewatembelea aweze kupumzika na kula chakula walichotayarisha. Mara nyingi wageni hupewa chai ya maziwa iliyochanganywa na chumvi kidogo.
Ubudha ni dini yenye washiriki wengi nchini Mongolia. Pia, kuna washiriki wa dini ya shaman, Uislamu, na Ukristo, na kuna idadi kubwa ya watu ambao hawana dini. Kuna Mashahidi wa Yehova zaidi ya 350 nchini Mongolia wanaofundisha Biblia watu zaidi ya 770.