Kupiga Picha Zinazofafanua Habari
Wapiga-picha wetu wanafaulu jinsi gani kupiga picha zinazoboresha machapisho yetu na kufafanua zaidi habari? Ili kuelewa hatua zinazohusika, ona jinsi jalada la gazeti la Amkeni! la Septemba 2015 lilivyopangwa na kutafutiwa picha. *
Ubunifu. Baada ya kusoma makala “Maoni Yenye Usawaziko Kuhusu Pesa,” wataalamu katika Idara ya Sanaa, iliyopo katika Kituo cha Elimu cha Watchtower huko Patterson, New York, waliandaa michoro kwa ajili ya habari hiyo. Kisha wakawapa ndugu wa Halmashauri ya Uandikaji ya Baraza Linaloongoza ambao walichagua picha ambayo itafaana na habari.
Mahali. Badala ya kwenda kwenye benki halisi, wapiga-picha wetu walitumia mojawapo ya mapokezi katika Kituo cha Elimu cha Watchtower kuonyesha mandhari ya benki. *
Wahusika. Wote waliopigwa picha ni Mashahidi wa Yehova na walichaguliwa ili waigize kama wateja wa kawaida wa benki katika jiji kubwa. Wapiga-picha huandika orodha ya majina ili watu walewale wasitumiwe sana katika machapisho yetu.
Vifaa. Idara ya Sanaa ilitafuta pesa za kigeni ili ionekane kana kwamba benki hiyo iko nje ya Marekani. Wapiga-picha walipanga vitu mbalimbali vinavyofaa ili kuhakikisha eneo hilo linafanana kabisa na benki. “Tunajitahidi kuhakikisha mambo yote ni halisi kabisa,” anasema mpiga-picha anayeitwa Craig.
Nguo na mapambo. Kwa ajili ya picha hiyo ya benki, wahusika walivaa nguo zao wenyewe. Lakini, kwa picha zinazohusisha hali za kihistoria au sare za pekee, idara hiyo ya sanaa inafanya utafiti na kushona nguo zinazofaa. Kuna watu wanaowapamba wahusika ili wapatane na muktadha, hali, au kipindi cha wakati kinachoonyeshwa kwenye picha. Craig anasema hivi, “Kwa sababu siku hizi kamera zinanasa picha za hali ya juu, tunahitaji kuwa makini sana. Hata kasoro ndogo inaweza kuharibu picha.”
Wakati wa kupiga picha. Wapiga-picha walihakikisha mwangaza ndani ya benki ulionyesha kwamba picha ilipigwa mchana. Kila wanapopiga picha, lazima wapiga-picha wahakikishe kwamba mwanga unafaa (kuonyesha mwangaza wa jua, mwezi, au mwangaza wa taa), ili ufaane na mazingira yanayopigwa picha, na upatane na hisia zinazoonyeshwa kwenye picha. Craig anasema, “Tofauti na video, picha hiyo moja tu inapaswa ionyeshe hisia za makala yote waziwazi, kwa hiyo mwanga ni muhimu sana.”
Kuhariri. Baadaye, wahariri wa picha walifanya maandishi juu ya pesa yasionekane waziwazi ili wasomaji wakazie fikira watu na si nchi ya pesa hizo. Ingawa mlango na fremu ya madirisha ilikuwa na rangi nyekundu, wahariri hao waliigeuza rangi ikawa ya kijani kibichi na hivyo kuipatanisha na rangi nyingine kwenye picha hiyo.
Mbali tu na Patterson, picha hupigwa katika ofisi nyingine za tawi ulimwenguni, kama vile Afrika Kusini, Australia, Brazili, Japani, Kanada, Korea, Malawi, Mexico, na Ujerumani. Katika maeneo hayo kuna wapiga-picha maalumu wanaoweza kuombwa waandae picha kwa ajili ya machapisho yetu. Kila mwezi, Idara ya Sanaa huko Patterson inakusanya picha 2,500 hivi. Picha nyingi kati ya hizo zinatumiwa kwenye magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni!, nakala zaidi ya milioni 115 za kila gazeti zilisambazwa katika mwaka wa 2015. Unakaribishwa kutembelea ofisi zetu Patterson, New York, au katika mojawapo ya ofisi zetu za tawi ulimwenguni pote ili upate habari zaidi.
^ fu. 2 Picha nyingi hupigwa kuliko zile zinazohitajiwa kwenye jalada. Hata hivyo, picha za ziada zinahifadhiwa kwenye maktaba ya picha na kutumiwa baadaye.
^ fu. 4 Ikiwa picha zinapigwa kwenye mtaa wa jiji, Idara ya Sanaa lazima kwanza ipate vibali kutoka kwa wenye mamlaka, itaje kihususa ni watu wangapi watahusika, vifaa vingapi vitahitajiwa, na ni mwanga wa aina gani utakaotumiwa.